Kamanda wa IRGC: Iran itajibu vikali kosa lolote la kimahesabu la adui
Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kuwa kitendo chochote cha uchokozi kutoka kwa adui kitakabiliwa na jibu kali na thabiti kutoka kwa vikosi vya ulinzi vya Iran.
Brigedia Jenerali Mohammad Karami ameyasema hayo siku ya Alhamisi wakati wa ziara yake katika visiwa vya Ghuba ya Uajemi kusini mwa Iran.
Amesema: “Kwa kutegemea irada ya Mwenyezi Mungu na kuungwa mkono na taifa shupavu, macho na lililo imara katika uwanja wa mapambano, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vitatoa jibu kali kwa mahesabu yoyote mabaya ya adui.”
Wakati huo huo, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Artesh) limesema kuwa meli za kivita za Marekani ziko mbali na pwani ya Iran kutokana na nguvu na uimara wa vikosi vya wanamaji vya Iran. Jeshi hilo limekanusha vikali madai ya Marekani kwamba uwezo wa kijeshi wa Iran umedhoofishwa au kuangamizwa.
Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia, Msemaji wa Jeshi, amesema kuwa vikosi vya wanamaji vya Iran vingali vinashika doria katika Bahari ya Oman, Bahari ya Kiarabu, na kaskazini mwa Bahari ya Hindi. Aidha amesema: “Iwapo, kama anavyodai [Rais wa Marekani Donald] Trump, Jeshi la Wanamaji lingekuwa limeangamizwa, basi adui angekaribia pwani zetu, lakini hawathubutu kabisa kufanya hivyo.”
Kauli yake ilikuja kama jibu kwa madai ya mara kwa mara ya Trump kuhusu kuharibiwa kwa majeshi ya Iran. Jenerali Akraminia ameyataja madai hayo kuwa ni ya uongo mtupu na kusisitiza: “Tupo uwandani katika eneo hili na tunalidhibiti kikamilifu.”
Aidha mnamo Septemba 9, msemaji wa IRGC alisema kwamba meli za kivita za Marekani zimerudi nyuma umbali wa angalau kilomita 400 kutoka Lango Bahari la Hormuz, na kwamba hakuna manowari yoyote ya Marekani iliyobaki ndani ya Ghuba ya Uajemi.
Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zilianzisha vita vyao haramu vya uchokozi dhidi ya Iran mnamo Februari 28 kwa kumuua kigaidi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, pamoja na makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi.
Siku arobaini baadaye, mnamo Aprili 8, maadui walilazimika kukubali kusitisha mapigano kufuatia muqawama na kusimama kidete majeshi ya Iran kupitia operesheni zake za kulipiza kisasi zilizofanikiwa, pamoja na udhibiti madhubuti wa Lango-Bahari la Hormuz.
Mnamo mwezi Julai, Marekani ilitekeleza mashambulizi mfululizo ya anga ya kikatili nchini Iran na kuweka mzingiro wa majini dhidi ya nchi hii, ikiwa ni ukiukaji wa Hati ya Makubaliano ya Islamabad (MoU) iliyotiwa saini na marais wa Iran na Marekani mnamo Juni 17 ili kuhitimisha vita.
Kama jibu la ukiukaji huo, majeshi ya Iran yalianzisha mashambulizi makali na yenye maangamizi makubwa dhidi ya shabaha za kimkakati za Marekani kote Asia Magharibi na kutangaza kufungwa kikamilifu kwa Lango-Bahari La Hormuz kwa shughuli zote za usafirishaji wa vyombo vya baharini.