Federica Mogherini: Iran imetekeleza makubaliano ya JCPOA
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana na ahadi zake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yaliyofikia baina yake na kundi la 5+1.
Federica Mogherini amesema hayo baada ya kikao cha pamoja cha Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na mawaziri wa nchi zinazounda kundi la 5+1 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na kuwaambia waandishi wa habari kwamba, Iran imetekeleza ahadi zake mkabala na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kama ninavyomnukuu:
"Tumepokea ripoti tatu za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomia (IAEA) ambazo zote zinathibitisha kwamba, Iran imechukua hatua zote ambazo ilipaswa kuzichukua kuhusiana na kadhia ya nyuklia."
Mogherini amesema pia kuwa, suala la makombora ya balestiki ya Iran halikujadiliwa katika kikao cha jana mjini New York na Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na wa kundi la 5+1 kwani majaribio hayo hayakiuki makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Zaidi ya mwaka mmoja umepita sasa tangu kuidhinishwe makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 na sasa utekelezaji wake umeingia katika mwezi wa tisa. Iran imetekeleza majukumu yake kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano hayo na suala hilo limethibitishwa pia na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).