Iran kwa Ujerumani: Katu hatutaacha kuiunga mkono Palestina
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katu nchi hii haitoacha kuiunga mkono Palestina.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika radiamali yake kwa matamshi ya Waziri wa Uchumi wa Ujerumani ambaye amesema kuwa uhusiano kati ya Berlin na Tehran unaweza kurejea katika hali ya kawaida na hata kuimarika zaidi iwapo Jamhuri ya Kiislamu itautambua utawala wa Kizayuni wa Israel.
Qassemi amesema uhusiano kati ya Iran na Ujerumani umejengeka katika misingi ya heshima na maslahi ya pande mbili na kusisitiza kuwa kutoa masharti ili kuimarisha uhusiano huo ni jambo lisilokubalika.
Katika mahojiano na gazeti la kila wiki la Der Spiegel,Sigmar Gabriel, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani alisema uhusiano wa Iran na Ujerumani unaweza kuimarika iwapo Tehran itatambua na kuheshimu uwepo wa Israel.
Gabriel ambaye anatazamiwa kuwasili hapa nchini Jumapili kwa ziara rasmi, aidha alisema ataibua suala la ukiukaji wa haki za binadamu hapa nchini katika ziara yake hiyo, kauli ambayo imekosolewa vikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye amesisitiza kuwa nchi hii hairuhusu nchi yeyote ya kigeni kuingilia masuala yake ya ndani.