Oct 04, 2016 04:45 UTC
  • IMF: Uchumi wa Iran unastawi kwa kasi baada ya JCPOA

Mfuko wa Fedha Duniani IMF umesema uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakuwa kwa kasi kubwa kufuatia kutekelezwa kwa makubaliano ya nyuklia unaofahamika kama Mpango Kamili ya Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Ripoti ya IMF iliyotolewa jana Jumatatu imesema kuwa, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza baada ya taifa hili kuondolewa vikwazo, uchumi wake umekuwa kwa kiwango kikubwa na cha kuridhisha. Kadhalika ripoti hiyo ya Mfuko wa Fedha Duniani imesema hatua ya Iran ya kuongeza kiwango cha uzalishaji na uuzaji wa mafuta nje ya nchi imesaidia kudhibiti kuporomoka kwa bei ya mafuta duniani.

IMF: Uchumi wa Iran utakuwa kwa 4.5% kati ya 2016-17

Aidha ripoti hiyo ya IMF imesema kuimarika sekta za kilimo, biashara na uchukuzi hapa nchini, kumechangia pakubwa katika ustawi wa uchumi wa Iran katika muda mfupi wa kuondolewa vikwazo nchi hii, kwenye sekta zingine zisizokuwa za mafuta.

Ali Akbar Salehi, Makamu wa Rais wa Iran

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni, Ali Akbar Salehi, Makamu wa Rais wa Iran, ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki alisema uchumi wa taifa hili unategemea uwezo wa ndani na unaelekea kwenye kilele cha ustawi na kwamba yote yamechangiwa na rasilimali ya vijana weledi na mahiri; na muhimu zaidi ya yote ni taifa hili kuwa na amani, uthabiti na usalama licha ya machafuko na ukosefu wa amani unaoshuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Tags