Iran yalaani mauaji ya Waislamu siku ya Ashura Nigeria, Afghanistan
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wamejumuika kwa ajili ya maombolezo ya Ashura, katika miji ya Kaduna na Funtua nchini Nigeria hapo jana.
Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesema kuna haja kwa wahusika wa jinai hiyo wafikishwe mbele ya sheria huku akivitaka vyombo vya usalama katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kuwadhaminia usalama waombolezaji hao wa Kiislamu badala ya kuwahujumu.
Watu 11 waliuawa jana baada ya jeshi la Nigeria kushambulia mkusanyiko wa Waislamu waliokuowa katika maombolezo ya Ashura na shughuli ya kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Aidha makumi ya Waislamu wengine wakiwemo watoto wadogo walikamatwa na polisi ya Nigeria wakati wa tukio hilo.
Hii sio mara ya kwanza kwa jeshi la Nigeria kuwashambulia Waislamu wa madhehebu ya Shia waliojumuika katika marasimu ya kidini. Disemba mwaka jana 2015, jeshi hilo liliwashambulia Waislamu wa mji wa Zaria jimboni Kaduna na kuua mamia miongoni mwao, mbali na kumtia nguvuni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky, baada ya kumpiga risasi kadhaa.
Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amelaani hujuma za kigaidi zilizolenga waombolezaji wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume SAW, katika mkoa wa Balkh na mji wa Kabul nchini Afghanistan, ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.