Mauzo ya mafuta ya Iran barani Asia yaongezeka kwa 92%
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i18445-mauzo_ya_mafuta_ya_iran_barani_asia_yaongezeka_kwa_92
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema uuzaji wa mafuta yake katika nchi za bara Asia umeongezeka na kufikia asilimia 92, kiwango kinachokaribia cha kabla ya vikwazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2016 04:27 UTC
  • Mauzo ya mafuta ya Iran barani Asia yaongezeka kwa 92%

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema uuzaji wa mafuta yake katika nchi za bara Asia umeongezeka na kufikia asilimia 92, kiwango kinachokaribia cha kabla ya vikwazo.

Wizara ya Mafuta ya Iran imesema iliuza mapipa milioni 1.7 ya mafuta ghafi kwa siku, barani Asia mwezi Agosti mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 92.

Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kuwa, wateja wa mafuta wa Iran barani Asia walinunua mapipa milioni 1.6 kwa siku, mwezi Julai mwaka huu, kiwango ambacho ni sawa na ongezeko la asilia 60 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Mafuta ghafi ya Iran

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, asilimia 63 ya mauzo ya mafuta yanayofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi, huelekea barani Asia; huku China na India zikiongoza orodha ya wateja wakuu wa Iran.

Haya yanajiri siku chache baada ya Bijan Namdar Zangeneh, Waziri wa Mafuta wa Iran kusema kuwa, kiwango cha uzalishaji mafuta ya Iran ni karibu mapipa milioni nne kwa siku hivi sasa na hii ina maana ya kukaribia mno kiwango cha uzalishaji wa mafuta ya Iran kabla ya kuwekewa vikwazo vya kidhulma na madola ya Magharibi kwa sababu ya miradi yake ya amani ya nyuklia.

Bijan Namdar Zangeneh, Waziri wa Mafuta wa Iran

Mapema mwezi huu wa Oktoba, Mfuko wa Fedha Duniani IMF ulisema kwamba, uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakuwa kwa kasi kubwa kufuatia kutekelezwa makubaliano ya nyuklia yanayofahamika kama Mpango Kamili ya Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).