Zarif: Kadhia ya Palestina ndio suala kuu kwa Ulimwengu wa Kiislamu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Muhammad Javad Zarif amesema kadhia ya Palestina ndio suala kuu kwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Dakta Zarif ameyasema hayo leo mji mkuu wa Lebanon, Beirut mbele ya hadhara ya viongozi wa makundi ya muqawama ya Palestina na kusisitiza kwamba Palestina ndio mhimili mkuu wa siasa za nje za Iran na siasa hizo zinafuatiliwa kwa uzito mkubwa na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Huku akiashiria kwamba leo hii kuna hatari mbili kuu zinazotishia eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa jumla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hatari kubwa zaidi kwa eneo na dunia ni utawala wa Kizayuni; na balaa hilo lililoletwa na Ukoloni ndio chanzo cha vitisho vyote dhidi ya amani, usalama na haki za binadamu.
Zarif ameongeza kuwa kutokana na utawala wa Kizayuni kumiliki vichwa visivyopungua 200 vya nyuklia na kutekeleza siasa vamizi pamoja na kukiuka kanuni zote za kimataifa, ndio adui hatari zaidi wa haki za binadamu; na kwamba utawala huo hauna mfano wake katika ushari na uovu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameutaja ugaidi wa kitakfiri kuwa ndio hatari kubwa ya pili inayoikabili jamii ya wanadamu na kufafanua kuwa ugaidi wa kitakfiri umezusha vita na machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati lakini magaidi hao hawajawa tishio wala kusababisha hatari yoyote kwa Israel.../