Iran yaikosoa Saudia kwa kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema mwenendo wa utawala wa Saudi Arabia kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu kwa maslahi yake ya kisiasa ni hatari na utakaowatumbukia nyongo karibuni hivi.
Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran aliyasema hayo jana Jumanne akijibu madai ya kipropaganda yaliyotolewa na utawala wa Aal-Saud kwamba, wapiganaji wa Yemen walishambulia kwa kombora mji mtakatifu wa Makka. Qassemi amesema madai hayo ya watawala wa Riyadh ni propaganda ambazo mtu yeyote katika dunia ya sasa hawezi kuziamini.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kutoa madai yasiyokuwa na msingi dhidi ya Yemen ni moja ya mbinu zinazotumiwa na Riyadh kutafuta uungwaji mkono na nchi za Kiislamu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, wapiganaji wa Yemen walifyatua kombora la balastiki lililolenga uwanja wa ndege wa Jeddah, lakini utawala wa kifalme wa Aal-Saud ukaeneza propaganda na uongo kupitia vyombo vya habari kwa kudai kwamba lengo la Wayemen ni kuulenga mji mtukufu wa Makka.
Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen alisema madai ya Saudi Arabia kwamba Sana'a imeushambulia kwa kombora mji mtakatifu wa Makka ni ishara ya kushindwa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Riyadh pamoja na waitifaki wake.