Ripoti ya Amano yathibitisha utendaji wa Iran katika utekelezaji wa JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i2065-ripoti_ya_amano_yathibitisha_utendaji_wa_iran_katika_utekelezaji_wa_jcpoa
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amewasilisha ripoti yake kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran baada ya kutekelezwa mpango wa JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2016 22:55 UTC
  • Ripoti ya Amano yathibitisha utendaji wa Iran katika utekelezaji wa JCPOA

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amewasilisha ripoti yake kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran baada ya kutekelezwa mpango wa JCPOA.

Mkurugenzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia ameeleza kuhusu matokeo ya uhakiki katika miradi ya nyuklia ya Iran kupitia ripoti yake ya Ijumaa aliyoiwasilisha kwa Bodi ya Magavana ya IAEA. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa masuala yote yaliyoafikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 yametekelezwa katika fremu ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kwa mujibu wa ramani ya njia.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa Iran imechukua hatua zinazohitajika katika kutekeleza ahadi za makubaliano kuhusiana na masuala ya nyuklia kuanzia siku ulipopasishwa mpango wa JCPOA hadi utekelezaji wake.

Kiujumla ripoti ya Amano imethibitisha hatua muhimu ambazo Iran imekuwa ikizitekeleza tokea tarehe 16 mwezi Januari kuhusu mpango huo.

Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kwa Bodi ya Magavana na kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa wakati mmoja inahusiana na hatua zilizochukuliwa na Iran katika fremu ya mpango wa JCPOA. Tarehe 20 Julai mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2231 ambalo lilimtaka Mkurugenzi Mkuu afanye uhakiki na kuchukua hatua zinazohitajika kuhusiana na ahadi za Iran kuhusu miradi yake ya nyuklia katika kutekeleza mpango wa JCPOA.

Kwa mujibu wa azimio hilo, Bodi ya Magavana ya wakala wa IAEA tarehe 25 mwezi Agosti mwaka jana ilimruhusu Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo kufanya uhakiki na kuchukua hatua za lazima kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran ambazo zimeshurutishwa katika mpango wa JCPOA.

Bodi hiyo tarehe Nane Machi mwaka 2006 ilipeleka faili la miradi ya nyuklia ya Iran katika Baraza la Usalama; ambapo baadaye maazimio sita yalipasishwa dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa maazimio yaliyowasilishwa chini ya kifungu cha Saba cha Hati ya umoja huo, mradi wa urutubishaji urani nchini Iran ulitambuliwa kama tishio kwa usalama na amani ya kimataifa, madai ambayo bila shaka yalitolewa kwa malengo ya kisiasa. Hata hivyo faili hilo la Iran hatimaye limefungwa katika fremu ya utekelezaji wa ramani ya njia kati ya Iran na Wakala wa IAEA, na maazimio yote ya huko nyuma ya Bodi ya Magavana yameondolewa. Hivi sasa masuala yote ya huko nyuma yamehitimishwa kwa mujibu wa ramani ya njia, na katika kalibu ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 kufuatia kuwasilishwa ripoti ya wakala wa IAEA. Kufikiwa makubaliano ya nyuklia kumesambaratisha njama za maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Iran tayari imeondolewa katika kifungu cha Saba cha Hati ya Umoja wa Mataifa. Iran wakati huhuo imepata haki yake yake ya kuendelea kurutubisha urani, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkubwa wa nchi kadhaa wanachama wa Barza la Usalama. Azimio la Bodi ya Magavana kwamba miradi ya nyuklia ya Iran ni ya malengo ya amani, limepelekea kutambuliwa mafanikio hayo. Kwa msingi huo Mpango Kamili wa Utekelezaji (JCPOA) unatambuliwa kuwa ni mafanikio licha ya kuwepo baadhi ya mapungufu na udhaifu. Kwa mujibu wa mpango wa JCPOA, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni nchi yenye miradi ya nyuklia inayotekelezwa kwa malengo ya amani, inamiliki pia kinu kamili cha mafuta huku haki yake ya kurutubisha urani ikitambuliwa. Mafanikio ambayo yanatajwa kama ushindi wa kisiasa.