Iran Kuchukua hatua kali kuhusu ukiukwaji wa mapatano ya nyuklia
(last modified Tue, 06 Dec 2016 05:58:34 GMT )
Dec 06, 2016 05:58 UTC
  • Iran Kuchukua hatua kali kuhusu ukiukwaji wa mapatano ya nyuklia

Iran itachukua hatua kali na imara iwapo kutakuwepo ukiukwaji wowote wa mapatano ya nyuklia baina yake na madola sita makubwa duniani.

Akizungumza Vienna Austria Jumatatu, Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran aidha amebainisha masikitiko yake kufuatia kile alichokitaja kuwa ni ‘hatua zisizo za hekima’ za Marekani dhidi ya mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama ‘Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).

Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilitia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA  Julai mwaka jana na kuanza kuyatekeleza Januari mwaka huu.

Akihutubu katika Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Nyuklia mjini Vienna, Salehi  amebaini kuwa Iran imekuwa ikifungamana na majukumu yake katika mapatano hayo ya nyuklia na wala haitachukua hatua ya kuyakiuka. Hata hivyo ameonya kuwa kuendelea kuwepo JCPOA kunategemea utekelezwaji wa ahadi za upande wa pili.

Salehi ametoa tamko hilo kufuatia hatua ya Alhamisi iliyopita ya Baraza la Senate la Marekani ya kurefesha vikwazo vya upande mmoja vya nchi hiyo dhidi ya Iran, hatua ambayo Iran imeitaja kuwa ni kinyume cha mapatano ya nyuklia.

Kwingineko katika hotuba yake, Salehi amesema Iran inataka ulimwengu usio na silaha za nyuklia na amesisitiza umuhimu wa kufikiwa lengo hili katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kituo cha kuunda silaha angamizi za nyuklia za utawala haramu wa Israel

Salehi ameashiria hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukataa kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezwaji Silaha za Nyuklia NPT na kusema utawala huo ni chanzo cha wasiwasi mkubwa dhidi ya usalama wa eneo na dunia.

Aidha ametoa wito wa kuwepo ushirikiano zaidi wa kimataifa katika uga wa teknolojia ya nyuklia hasa usalama wa teknolojia hiyo.

Tags