Feb 29, 2016 02:33 UTC
  • Kiongozi alipongeza taifa la Iran kwa kushiriki kwa wingi katika chaguzi

Kiongozi Muadhamu wa Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza taifa la Iran kwa kushiriki kwa wingi katika chaguzi mbili za siku ya Ijumaa.

Katika ujumbe wake siku ya Jumapili, Ayatullah Ali Khamenei amesema, kwa kujitokeza kwa wingi katika chaguzi za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, na Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi, wananchi wa Iran wameuonyesha ulimwengu 'demokrasia ya kidini'.

Katika ujumbe wake huo, Kiongozi Muadhamu sambamba na kulipongeza taifa la Iran, amesema maafisa wa nchi wanapaswa kutekeleza kazi zao kwa ikhlasi ili kwa njia hiyo wawashukuru wananachi. Aidha amesisitiza kuhusu ustawi wa pande zote Iran kwa kutegemea vipawa vya ndani ya nchi.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Kiongozi Muadhamu amewakumbusha waliochaguliwa pamoja na maafisa wengine wa mihimili mikuu ya dola kuhusu umuhimu wa maisha yasiyo ya kifahari, uaminifu, kuzingatia maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi au ya kimrengo, kusimama kishujaa mbele ya uingiliaji wa madola ya kigeni, kuwa na misimamo ya kimapinduzi katika kukabiliana na maadui na wahaini na kuwa na muelekeo wa kijihadi. Ayatullah Khamenei amesema ustawi wa nchi ndiyo lengo kuu na kwamba haikubaliki kuwa na ustawi bandia ambao unakiuka heshima na uhuru wa kitaifa.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, ustawi haumaanishi kumwezwa na madola ya kiistikbari na kibeberu duniani.

Uchaguzi wa Bunge la Kumi la Iran na Baraza la Tano la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 26 Februari. Matokeo kamili ya uchaguzi huo yanatazamiwa kutangazwa baadaye Jumatatu.

Tags