Iran na Indonesia kuimarisha usalama katika ulimwengu wa Kiislamu
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na Indonesia zina nafasi ya kipekee ya kuimarisha usalama katika eneo na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.
Dakta Rouhani amesema hayo hii leo mjini Tehran, katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Indonesia, Joko Widodo. Amesema Iran inathamini uhusiano wake na Indonesia na kusisitizia umuhimu wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa pande mbili katika nyuga mbali mbali kwa lengo la kuboresha usalama na uthabiti sio tu katika eneo, bali katika nchi zote za Kiislamu.
Baada ya kusaini hati 4 za makubaliano ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara, Rais wa Iran amesema nchi hii itafanya muamala wa kibiashara na Indonesia kwa kuiuzia mafuta ghafi, gesi na bidhaa nyinginezo za petrokemikali.
Rais Hassan Rouhani na mwenzake wa Indonesia Joko Widodo wamefanya mazungumzo ya pande mbili huku masuala ya kuimarisha ushirikiano wa pamoja katika nyanja mbalimbali kati Tehran na Jakarta kieneo na kimataifa; na vile vile kuimarishwa uhusiano kati ya Tehran na Jakarta katika nyanja mbalimbali kukiwa katika masuala yaliyojadiliwa katika mazungumzo ya marais hao.
Kadhalika pande mbili hizo zimejadili masuala ya ulimwengu wa Kiislamu, na migogoro katika nchi za Yemen, Syria na Myanmar.
Rais wa Indonesia aliwasili jana Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kwa shabaha ya kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Iran.