Mufti Mkuu wa Syria aishukuru Iran kwa misaada yake
Mufti Mkuu wa Syria ameishukuru Iran kwa misaada yake kwa wakazi wa mji wa Halab (Aleppo) kaskazini mwa Syria.
Akizungumza leo katika Mkutano wa 30 Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran,Sheikh Ahmad Badruddin Hasun Mufti Mkuu wa Syria ameishukuru Iran kwka misaada yake kwa Syria katika kupambana na mirengo ya kitakfiri na kueleza kuwa, Iran ya Kiislamu chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu, wananchi na serikali imeweza kuwasaidia wananchi wa Syria.
Mufti Mkuu wa Syria ameashiria jukumu kubwa la maulamaa wa Ulimwengu wa Kiislamu na kueleza kuwa, misaada ya Iran na Lebanon imethibitisha kuwa, moto uliowashwa hivi sasa katika Ulimwengu wa Kiislamu hautokani na sababu za kimadhehebu, bali ni vita vya mabeberu wa dunia na wakoloni dhidi ya Waislamu; na kwa msingi huo amesema maulamaa wanapasa kuwa macho kuhusiana na suala hilo.
Mkutano wa 30 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza leo hapa Tehran kwa kaulimbiu ya "Umoja na Udharura wa Kukabiliana na Makundi ya Kitakfiri". Mkutano huu utaendelea kwa siku tatu hapa Tehran. Wageni wa Kiirani na kutoka nje ya nchi zaidi ya 300 wanashiriki katika mkutano huo lengo likiwa ni kuchunguza kadhia mbalimbali kama vile udharura wa kupambana na mirengo ya kitakfiri.