Ayatullah Siddiqi: Kukombolewa Aleppo ni ushindi kwa Waislamu wote duniani
Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Tehran amepongeza wanajeshi wa Syria na vikosi vya vya kujitolea vya wananchi kwa kuukomboa mji wa Aleppo (Halab) uliokuwa ukishikiliwa na magaidi huko kaskazini mwa Syria, na kubainisha kuwa, ushindi huo sio tu wa taifa la Syria bali ni ushindi pia kwa Waislamu wote duniani.
Akizungumza katika hotuba za Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa Tehran, Ayatollah Kadhim Siddiqi amesema ukombozi huo umetokana na damu za mashahidi waliojitolea muhanga katika mapambano dhidi ya magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya Kiistikbari.
Hujjatul Islam wal Muslimin Siddiqi amesema wanamuqawama na jeshi la nchi hiyo wamezishinda Marekani na Saudia kwa kupata ushindi dhidi ya magaidi na utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa, ushindi huo ni wa kiutamaduni na kiidiolojia na pia ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyosambaratisha njama za mabeberu.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran amefafanua kuwa, wanamuqawama wamepata ushindi huo kutokana na kusimama kwao kidete, kutobabaishwa, na kumtegemea Mwenyezi Mungu, na ndipo wamefanikiwa kuvunja njama za maadui licha ya utajiri mkubwa wa fedha na silaha wa madola ya kibeberu yaliyokuwa yakiunga mkono harakati za magaidi hao kwa hali na mali.
Ayatullah Kadhim Siddiqi, Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran ameongeza kuwa, kukombolewa Halab ni pigo kwa magenge ya kigaidi na waungaji mkono wao katika eneo.
Taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi na jeshi la Syria ilitangaza habari ya kukombolewa kikamilifu mji wa Aleppo toka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS.
Jeshi la Syria limesema mji wa Halab ambao uko kaskazini mwa Syria hivi sasa umesafishwa kikamilifu baada ya magaidi kuangamizwa, baadhi yao kufurushwa na wengine kujisalimisha. Mara baada ya kutangazwa kukombolewa kikamilifu mji wa Halab, wananchi wa nchi hiyo walimiminika barabarani na kufanya sherehe usiku wa kuamkia leo.
Hapo jana Rais Bashar al-Assad wa Syria alisema kukombolewa kikamilifu mji wa kistratejia wa Aleppo (Halab), kaskazini magharibi mwa nchi ni ushindi mkubwa sio tu kwa taifa hilo, bali pia kwa Iran na Russia.