Velayati: Wapinzani wabeba silaha wa Syria hawatoshirikishwa katika mazungumzo ya Astana
Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratjia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran amesema, wapinzani wabeba silaha wa Syria hawatoshirikishwa katika mazungumzo yajayo ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo yaliyopangwa kufanyika katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana.
Ali Akbar Velayati, ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya mazungumzo aliyofanya na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem hapa mjini Tehran hapo jana.
Velayati amefafanua kuwa, mazungumzo ya Astana yatashirikisha wapinzani ambao wameyakubali mamlaka ya kujitawala ya ardhi yote ya Syria pamoja na utawala wa kisheria wa nchi hiyo.
Dakta Velayati amesisitiza kuwa, mazungumzo yaliyofanyika baada ya ushindi wa kukombolewa mji wa Halab baina ya maafisa wa sera za nje na wa usalama wa Syria na Iran na ushirikiano uliopo kati ya Iran na Syria na pia kati ya Iran, Russia na Syria una umuhimu mkubwa.
Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratijia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran ameongeza kuwa, ushindi wa Syria na waitifaki wake katika mji wa Halab ni ushindi mkubwa zaidi kushuhudiwa katika historia ya zama hizi ya eneo la Mashariki ya Kati.
Usitishaji vita wa nchi nzima ulianza kutekelezwa nchini Syria tangu siku ya Ijumaa iliyopita, lakini baadhi ya makundi yanayobeba silaha yamekiuka makubaliano hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid al-Muallem aliwasili mjini Tehran juzi Jumamosi na tayari ameshakutana na kufanya mazungumzo na Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran…/