Dakta Veleyati: Katu Iran haitolitelekeza taifa la Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i22807-dakta_veleyati_katu_iran_haitolitelekeza_taifa_la_syria
Ali Akbar Velayati, Mshauri Mkuu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amesema hakuna siku Jamhuri ya Kiislamu itawatelekeza wananchi na serikali ya Syria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 04, 2017 04:09 UTC
  • Dakta Veleyati: Katu Iran haitolitelekeza taifa la Syria

Ali Akbar Velayati, Mshauri Mkuu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amesema hakuna siku Jamhuri ya Kiislamu itawatelekeza wananchi na serikali ya Syria.

Dakta Veleyati aliyasema hayo jana Jumanne hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Nouri al-Maliki, Makamu wa Rais wa Iraq na kubainisha kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuindoa Iran katika misingi ya sera yake ya kuunga mkono muqawama na harakati za mapambano, wakiwemo wananchi na serikali ya Syria.

Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu

Amesisitiza kuwa, juhudi za kupatikana amani na uthabiti zinazofanywa na Iran na Russia zinafanyika kwa ushirikiano wa karibu na serikali ya Damascus na kuongeza kuwa, hakuna nchi inayoruhusiwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu ambayo imekuwa kwenye mgogoro na machafuko kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Dakta Veleyati ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratijia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran ameongeza kuwa, ushindi wa Syria na waitifaki wake katika mji wa Halab ni ushindi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama hizi ya eneo la Mashariki ya Kati na kwamba wananchi wa Syria ndio watakaoamua wenyewe mustakabali wa nchi yao.

Nouri al-Maliki, Makamu wa Rais wa Iraq

Amefafanua kuwa, usitishaji vita wa nchi nzima ulianza kutekelezwa nchini Syria tangu Ijumaa iliyopita, lakini baadhi ya makundi yanayobeba silaha yamekiuka makubaliano hayo yakifahamu fika kuwa yana rekodi nyeusi katika nchi hiyo.