Mali yasema msimamo wake na Iran ni mmoja kuhusu kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i23287-mali_yasema_msimamo_wake_na_iran_ni_mmoja_kuhusu_kadhia_ya_palestina
Rais wa Bunge la Kitaifa la Mali amesema msimamo wa nchi yake kuhusu kadhia ya Palestina unafanana na wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na amekashifu mienendo ya Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hilo la Kiarabu kwa miaka kadhaa sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2017 12:00 UTC
  • Mali yasema msimamo wake na Iran ni mmoja kuhusu kadhia ya Palestina

Rais wa Bunge la Kitaifa la Mali amesema msimamo wa nchi yake kuhusu kadhia ya Palestina unafanana na wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na amekashifu mienendo ya Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hilo la Kiarabu kwa miaka kadhaa sasa.

Issaka Sidibe, Rais wa Bunge la Taifa la Mali ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran leo Jumatano, akiwa pamoja na Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Ali Larijani na kubainisha kuwa, matatizo wanayoyapitia wananchi wa Palestina yanaitiwa wasiwasi mkubwa nchi yake.

Ameongeza kuwa, serikali ya Bamako inaunga mkono kikamilifu azimio lililopasishwa hivi karibuni na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likilaani na kutaka kusitishwa mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu huku akitilia mkazo kuwa Mali itahudhuria kongamano la kuunga mkono Palestina linalotazamiwa kufanyika nchini Iran mwezo ujao wa Februari.

Sidibe na Larijani kabla ya kuwahutubia waandishi wa habari mjini Tehran

Kadhalika Rais wa Bunge la Kitaifa la Mali amesema binafsi atazungumzia changamoto zinazoukabili uliwengu wa Kiislamu katika duru ya 12 ya Mkutano wa Umoja wa Mabunge ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) hivi karibuni.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Iran, Ali Larijani amesema Tehran na Bamako zina msimamo pacha ikija katika suala la kujaribu kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazozikabili nchi za Kiislamu, haswa kadhia ya Palestina.

Amebainisha kuwa, Mali ni nchi yenye ushawishi mkubwa barani Afrika, na mazungumzo kati ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za uchumi, biashara na utamaduni yamekuwa yakifanyika mara kwa mara. 

Issaka Sidibe, Rais wa Bunge la Kitaifa la Mali ambaye aliwasili nchini leo asubuhi akiongoza ujumbe wa wabunge kwa ajili ya ziara ya siku mbili ya kikazi, anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali ya Tehran kabla ya kuondoka nchini kesho Alkhamisi akirejea Bamako.