Ayatullah Larijani: Maadui wanaogopa Iran kuwa kigezo kwa Waislamu bilioni moja
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i24751-ayatullah_larijani_maadui_wanaogopa_iran_kuwa_kigezo_kwa_waislamu_bilioni_moja
Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran amesema kuwa wahka na wasiwasi mkubwa wa maadui unatokana na kuiona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa kigezo na ruwaza njema kwa Waislamu zaidi ya bilioni moja duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2017 23:45 UTC
  • Ayatullah Larijani: Maadui wanaogopa Iran kuwa kigezo kwa Waislamu bilioni moja

Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama nchini Iran amesema kuwa wahka na wasiwasi mkubwa wa maadui unatokana na kuiona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa kigezo na ruwaza njema kwa Waislamu zaidi ya bilioni moja duniani.

Ayatullah Sadiq Amoli Larijani ambaye alikuwa kihutubia kongamano la Mfumo wa Kiibeberu wa Mrengo wa Vibaraka uliofanyika jana mjini Tehran amesema kuwa, moja ya sababu za sisitizo la mfumo wa kibeberu wa kutaka kupenya na kuingia nchini Iran ni wasiwasi wake wa kuiona Jamhuri ya Kislamu ikiwa kigezo bora na chenye taathira kubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Ayatullah Larijani amesema kuwa, mfumo wa kibeberu unaitambua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mpinzani wake wa kifikra na kivitendo ambaye uhai wake umesimama kwenye misingi ya Tauhidi na mafundisho ya Qur'ani.

Ayatullah Sadiq Larijani

Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama vya Iran ameongeza kuwa, utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umejengwa kwa mujibu wa mtazamo wa Qur'ani na itikadi ya Tauhidi na umekuwa chanzo cha kheri na baraka, suala ambalo linawatia woga maadui.

Kuhusu woga na wasiwasi wa nchi za Magharibi mkabala wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon na madai yao ya kuituhumu harakati hiyo kuwa ni ya kigaidi, Ayatullah Sadiq Larijani amesema kuwa, Hizbullah na makundi mengine ya Kiislamu ya Yemen na Iraq yaliundwa kwa mujibu mafundisho ya Kiislamu.