Wapalestina: Kama si msaada wa Iran, kadhia yetu ingelikuwa imesahauliwa
Makundi mbalimbali ya Palestina yamesisitiza kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umelisaidia mno taifa la Palestina na kuzuia kusahauliwa taifa hilo madhlumu.
Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo leo na kuanza kwa kumnukuu Ibrahim al Najjar, kiongozi wa ngazi za juu ya harakati ya Jihad al Islami ya Palestina akisema, katika wakati ambapo baadhi ya Waarabu walikuwa wanafanya njama za kufifiliza umuhimu wa suala la Palestina, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran uliibadilisha Palestina kuwa suala kuu la ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu.
Amesema, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameifanya kambi ya muqawama wa kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel iwe na nguvu zaidi kwani Wairani wanaihesabu Palestina kuwa ni medani ya kupambana na adui na wanaamini kuwa kupata ushindi Palestina ni sawa na kupata ushindi dini ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Ismail Ridhwan, kiongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Palestina HAMAS amesema, uungaji mkono wa kila upande wa Iran kwa kadhia ya Palestina ni nukta muhimu mno katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Kizayuni.
Naye Kayed al Goul, mjumbe wa Kamati Kuu ya Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina amesema, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamehuisha matumaini ya kujikomboa mataifa ya wanyonge duniani kutoka kwenye makucha ya madola ya kibeberu yanayouunga mkono kwa kila hali utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema, kushiriki kikamilifu Iran katika mapambano dhidi ya ubeberu wa Kizayuni-Kimarekani kumepelekea kupata uhai mpya Palestina ingawa hata hivyo kuna njama zinaendelea za kujaribu kuisahaulisha kadhia ya Palestina.
Baada ya kuendesha mapambano ya miaka mingi, hatimaye Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1979 na kwamba moyo wa taifa la Iran wa kujitolea na kukubali kuingia hatarini kwa ajili ya kuiletea heshima dini tukufu ya Kiislamu baada ya ushindi wa mapinduzi hayo matukufu, daima umekuwa ni nguzo madhubuti inayotegemewa na mataifa mengine yanayopigania ukombozi duniani.