Jeshi la Majini la Iran lafanyia majaribio kombora la topedo
Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo limefanyia majaribio yaliyofana kombora aina ya topedo katika siku ya mwisho ya mazoezi makubwa ya kijeshi katika maji ya kitaifa na kimataifa.
Mazoezi hayo yaliyoanza Jumapili yamepewa jina la Velayat 95 na yalikuwa yakifanyika katika eneo kubwa la baharini katika Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormoz, Bahari ya Oman na kaskazini mwa Bahari ya Hindi.
Kombora hilo la topedo lijulikanalo kama Valfajr limevurumishwa kutoka nyambizi ya Qadir ya Jeshi la Majini la Iran na limefanikiwa kuzamisha meli iliyokuwa imelengwa. Topedo ni aina ya kombora ambalo aghalabu hurushwa kutoka chini au juu ya maji kwa ajili ya kuzamisha vyombo vinavyosafiri baharini. Kombora hilo lina uwezo wa kwenda kwa kasi likiwa ndani ya maji.
Katika mazoezi hayo hiyo jana pia Jeshi la Majini la Iran lilifanyia majaribio yaliyofana kombora jipya zaidi la baharini lijulikanalo kama"Nassir".
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu, Admeri Habibollah Sayyari amesema kuwa lengo la mazoezi hayo ya kijeshi ni kupeleka ujumbe wa amani na urafiki kwa nchi za kanda hii, kuimarisha uwezo wa kujihami, kuzidisha kuwango cha usalama na kukabiliana na maharamia na ugaidi wa baharini.