Rais Rouhani: Tutaendeleza "uchumi wa muqawama" kwa nguvu zote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i26422-rais_rouhani_tutaendeleza_uchumi_wa_muqawama_kwa_nguvu_zote
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua zilizochukuliwa na serikali yake za kufanikisha "uchumi wa muqawama" unaotegemea uwezo wa ndani ya Iran ni nzuri na ameahidi kuimarisha miundombinu ya uchumi huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 15, 2017 13:03 UTC
  • Rais Rouhani: Tutaendeleza

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua zilizochukuliwa na serikali yake za kufanikisha "uchumi wa muqawama" unaotegemea uwezo wa ndani ya Iran ni nzuri na ameahidi kuimarisha miundombinu ya uchumi huo.

Amesema hayo leo Jumatano mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, kazi iliyofanyika hadi hivi sasa katika kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kutegemea bidhaa za ndani ni nzuri sana.

Amesema, miongoni mwa mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na serikali yake katika kipindi cha miezi 12 iliyopita (kipindi cha mwaka mmoja wa Kiirani wa 1395 Hijria Shamsia) ni pamoja na kuimarisha usalama nchini, kuendeleza miradi ya kiuchumi, kujitosheleza katika ngano, kupungua uzorotaji wa huko nyuma katika masuala ya nishati na kupatikana mafanikio mazuri katika uzalishaji wa chakula, kilimo, usafiri wa reli, barabara, anga na sekta ya utalii, sambamba na kuzinduliwa mabwawa na viwanda vingi vipya.

Rais Hassan Rouhani

 

Rais Rouhani aidha amesema, katika kipindi hicho cha miezi 12, serikali yake imeweza kupunguza kwa kiwango kikubwa kutegemea mafuta katika bajeti yake na kujikita zaidi katika mapato yanayotokana na kodi, kuzalisha bidhaa na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za ndani na nje ya Iran kwa kuimarisha sekta ya uchukuzi na kuifanya Iran kuwa moja ya vituo vikuu vya kusafirishia bidhaa za nchi za eneo hili.

Vile vile amesema, wananchi wa Iran wamekuwa pamoja na serikali muda wote katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kusisitiza kwamba, inabidi juhudi zaidi zifanyike kuhakikisha maendeleo zaidi yanapatikana katika nyuga zote hususan za kiuchumi.