Balozi: Kiongozi Muadhamu, Rouhani wanaupa umuhimu uhusiano wa Iran na Russia
Balozi wa Iran mjini Moscow amesema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais Hassan Rouhani wanaupa umuhimu mkubwa na wa kipekee uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Russia na wanataka kuuona ukiimarika.
Mehdi Sanaei, Balozi wa Iran nchini Russia aliyasema hayo jana Jumamosi, siku mbili kabla ya Rais Rouhani kuanza safari yake nchini Russia kesho Jumatatu, ambapo anatazamiwa kukutana na mwenzake Vladimir Putin.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran nchini Russia amefafanua kuwa, uhusiano wa Tehran na Moscow ni zaidi ya mahusiano ya pande mbili, kieneo na kimataifa, bali umekuwa kama kiigizo katika medani ya kimataifa.
Amesema mielekeo inayofanana ya Moscow na Tehran katika masuala mbalimbali kama vile ushirikiano dhidi ya ugaidi na kadhia ya Syria, inaashiria uhusiano maalumu kati ya nchi mbili hizi.
Rais Rouhani anatazamiwa kuwasili Moscow kesho Jumatatu katika ziara ya siku mbili, kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin wa Russia.
Wawili hao wanatazamiwa kushuhudia kusainiwa hati 10 za makubaliano ya ushirikiano sambamba na kuainisha ramani ya njia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa Tehran na Moscow.