Rouhani: Moja ya malengo ya uchumi wa muqawama ni kutotetereshwa kiuchumi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kusimama imara na kutotetershwa na mashinikizo ya nchi ajinabi ni moja ya malengo ya uchumi wa muqawama.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumatatu wakati alipokutana na maafisa wa serikali na wakurugenzi wa taasisi mbalimbali na kuutaja uzalishaji wa bidhaa za ndani kuwa ni mwanzo wa kupatikana ajira na mafanikio ya kiuchumi.
Rais Rouhani amebainisha kuwa, chini ya kivuli za kupatikana ajira na kuweko kasi ya uzalishaji, Iran itapiga hatua na kuweza kufanikisha malengo yote mawili yaliyobainishwa wazi na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uga wa uzalishaji na ajira kwa ajili ya mwaka huu mpya wa 1396 Hijria Shamsiya.
Rais Rouhani ameongeza kuwa, kufanyika jitihada za kuzalisha ajira humu nchini ni jukumu la kidini, kitaifa na kimapinduzi na kwamba, lengo la serikali katika mwaka huu wa 1396 Hijria Shamsiya ni kuona kunapatikana ajira mpya kwa ajili ya zaidi ya watu laki saba.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia makubaliano ya nyukia ya JCPOA na kueleza kuwa, lengo la Iran katika mpango huo ni kuona inafanikiwa kukata mnyororo wa vikwazo vya kidhulma na vya kutwishwa.
Vile vile amesisitiza kuwa, Iran ina imani na kura za wananchi katika uchaguzi na kwamba malengo makubwa ya wananchi wa iran yatafikiwa kupitia njia hiyo. Duru ya 12 ya uchaguzi wa Rais na duru ya 5 ya uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji vya Iran utafanyika tarehe 19 mwezi Mei mwaka huu.