Rouhani: Teknolojia ya Nyuklia ni dharura kwa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27512-rouhani_teknolojia_ya_nyuklia_ni_dharura_kwa_iran
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Teknolojia ya nyuklia ni dharura kwa taifa la Iran na sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kuendelelezwa hii teknolojia ni sisitizo sahihi."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 09, 2017 09:21 UTC
  • Rouhani: Teknolojia ya Nyuklia ni dharura kwa Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Teknolojia ya nyuklia ni dharura kwa taifa la Iran na sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kuendelelezwa hii teknolojia ni sisitizo sahihi."

Rais Hassan Rouhani wa Iran ameyasema hayo leo Jumapili mjini Tehran katika hafla ya Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia  na kuongeza kuwa nara ya 'Teknolojia ya Nyuklia Ni Haki Yetu ya Kimsingi" imefanikishwa katika uga wa kimataifa kutokana na udiplomasia wenye umahiri.

Rais Rouhani amesema kutekelezwa miradi 42 ya nyuklia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni natija ya usimamizi wa kijihadi na kimapinduzi na kuongeza kuwa: "Usimamizi wa kisayansi, kimapinduzi, kijihadi na kibasiji (kujitolea) ni mambo ambayo yamepelekea nishati ya nyuklia kudhihiri katika sekta mbali mbali za maisha ya watu wa Iran."

Rais Rouhani amesema kuwa, baadhi ya nchi duniani mnamo mwaka 2003 zilikuwa zikitaka kuipokonya Iran teknolojia ya nyuklia kwa visingizio mbali mbali na kuongeza kuwa: "Kusimama kidete mbele ya madola makubwa duniani katika mwaka huo kulipelekea faili la nyuklia la Iran lililokuwa katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki lisifikishwe katika Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa na suala hilo liliashiria ushindi wa taifa la Iran mbele ya Marekani."

Rais Rouhani akizindua mafanikio ya Iran katika teknolojia ya nyuklia, Tehran 09/04/2017

Rais wa Iran aidha amekosoa vikali hujuma ya Marekani dhidi ya Syria na kusema katika ulimwengu unaotawaliwa na undumakuwili, Marekani, pasina kuwepo idhini ya Umoja wa Mataifa imejipa haki ya kuishambulia nchi huru katika eneo nyeti la Mashariki ya Kati. Rais wa Iran amebainisha masikitikio yake kuwa baadhi ya nchi katika eneo zimeipongeza Marekani kwa kuvamia Syria kijeshi. Amesema wanaofurahia hujuma ya Marekani Syria wafahamu kuwa zamu yao nayo itafika tu. Rais Rouhani pia ameashiria uchaguzi ujao wa rais na mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji nchini Iran ambao umepangwa kufanyika Mei 19 na kusema: "Uchaguzi wa Iran si kama uchaguzi wa Marekani. Taifa la Iran kwa umoja na mshikamano wa kitaifa litaionyesha dunia nguvu ya nchi hii katika uchaguzi."