Wagombea urais Iran kuanza kujiandikisha leo
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Iran amesema kuwa, wagombea wa duru ya 12 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wataanza kujiandikisha rasmi leo Jumanne.
Bw. Ali Asghar Ahmadi alitangaza habari hio jana na kuongeza kuwa, uandikishaji huo wa wagombea wa urais utafanyika kwa muda wa siku tano na utaendelea hadi tarehe 15 mwezi huu wa Aprili.
Amesema, watu wote waliotimiza masharti ya kugombea wako huru kuandikisha majina yao katika ofisi za tume hiyo zilizoko kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran.
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na duru ya tano ya uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji unatarajiwa kufanyika tarehe 19 Mei mwaka huu.
Rais Hassan Rouhani anatarajiwa kutetea kiti chake hicho kwenye uchaguzi huo kuchuana na wagombea wengine wa mirengo tofauti.
Ikumbukwe kuwa uchaguzi nchini Iran unafanyika kwa uhuru kamili kiasi kwamba vyombo vya dola ni marufuku kuingilia masuala ya uchaguzi kama ambavyo vyombo vya habari vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinatoa haki sawa kwa wagombea wote kutangaza sera zao bila ya kujali cheo na nafasi ya mgombea katika jamii.