Iran kuandaa uchaguzi wa amani na wenye ushiriki mkubwa wa wananchi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27624-iran_kuandaa_uchaguzi_wa_amani_na_wenye_ushiriki_mkubwa_wa_wananchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Iran amesema uchaguzi ujao wa rais na mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji utakuwa wa amani, salama, wa kisheria na wenye ushiriki mkubwa wa wananchi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 11, 2017 03:12 UTC
  • Iran kuandaa uchaguzi wa amani na wenye ushiriki mkubwa wa wananchi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Iran amesema uchaguzi ujao wa rais na mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji utakuwa wa amani, salama, wa kisheria na wenye ushiriki mkubwa wa wananchi.

Abdul-Ridha Rahmani-Fadhli ameyasema hayo leo asubuhi hapa mjini Tehran mara baada ya kuanza zoezi la kuandikishwa wagombea wa uchaguzi wa rais wa Iran wa awamu ya 12 katika makao makuu ya tume ya uchaguzi nchini. Ameongeza kuwa, kwa mara nyingine, taifa adhimu la Iran litaunda hamasa kwa kujitokeza kwa wingi wananchi katika uchaguzi wa tarehe 19 mwezi ujao wa Mei.

Zoezi la kuandikisha wagombea kiti cha urais Iran

Zoezi la kuandikishwa wagombea kiti cha urais wa Iran limeanza leo asubuhi kwa amri ya Waziri wa Mambo ya Ndani. Wanaotaka kugombea wana fursa ya siku tano kuanzia leo hadi Jumamosi 15 Aprili kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki katika mchuano wa kiti cha urais.

Uchaguzi wa rais na ule wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji na pia uchaguzi mdogo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, utafanyika Mei 19.