Spika: Kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi kutawezesha kushindwa njama za maadui
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema uchaguzi ni jambo hasasi na jema na akasisitiza kwamba kushiriki kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi kutapelekea kushindwa njama za maadui.
Ali Larijani ameyasema hayo jana Jumamosi katika kongamano la 22 la kitaifa la makamanda, wakuu na wakurugenzi wa jeshi la Polisi lililofanyika hapa mjini Tehran. Ameongeza kuwa mahudhurio ya wananchi katika uchaguzi ndio nguzo na mhimili mkuu wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Dakta Larijani amebainisha kuwa uhamasishaji na ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi ni jambo muhimu na akaongezea kwa kusema: Jeshi la Polisi la Iran ni mhimili wa kuufanya uchaguzi uwe wa amani.
Spika wa Bunge ameuelezea utendaji wa jeshi la Polisi la Iran katika miaka ya karibuni kuwa ni chanya na wa mafanikio na akafafanua kwamba: Iran ina usalama thabiti katika eneo lenye migogoro la Mashariki ya Kati; na hilo limetokana na jitihada za vyombo vyote vya kudhamini amani na usalama nchini.
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ule wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji umepangwa kufanyika tarehe 19 Mei kote nchini.
Sayyid Mustafa Agha Mir Saliim, Is'haq Jahangiri Koshai, Hassan Rouhani, Sayyid Ebrahim Raeisi Sadati, Muhammad Baqir Qalibaf na Sayyid Mustafa Hashemi-taba ni wagombea sita waliopitishwa katika kinyangányiro cha kuwania urais.../