Umoja wa Ulaya wasisitiza kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28280-umoja_wa_ulaya_wasisitiza_kutekelezwa_kikamilifu_makubaliano_ya_nyuklia_ya_jcpoa
Umoja wa Ulaya umetaka kuwepo hakikisho kamili na athirifu la utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2017 03:28 UTC
  • Umoja wa Ulaya wasisitiza kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Umoja wa Ulaya umetaka kuwepo hakikisho kamili na athirifu la utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Helga Schmidt, Naibu Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ambaye anaongoza timu ya mataifa ya Ulaya katika kamisheni ya pamoja ya JCPOA ametoa taarifa na kutangaza kuwa washiriki wa kikao cha kamisheni hiyo wamesisitiza juu ya udharura wa kuwepo hakikisho na dhamana ya utekelezaji kamili na athirifu wa makubaliano hayo ya nyuklia.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kikao cha Vienna kilichofanyika jana kimetoa fursa  ya kuchunguza utekelezaji wa JCPOA kwa kuzingatia makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa na yanayohusiana na vikwazo.

Kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano ya JCPOA, kamisheni ya pamoja ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ndiyo yenye dhamana ya kusimamia utekelezaji makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Jamhuri ya Kiislamu na madola sita makubwa ya dunia.

Helga Schmidt (kushoto) na Mkuu wa timu ya Iran katika JCPOA Abbas Araqchi

Kikao cha saba cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA kimehudhuriwa na ujumbe wa Iran, nchi tano za kundi la 5+1 na mwakilishi mwandamizi wa Umoja wa Ulaya.

Tarehe 14 Julai 2015, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani zilisaini mkataba kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran ambao utekelezaji wake ulianza Januari 16 mwaka uliopita wa 2016.

Hata hivyo Marekani, ambayo ni mmoja wa wanachama wa kundi la 5+1 inakwepa kutekeleza ahadi zake na badala yake imekuwa ikichukua hatua ambazo zinakiuka makubaliano hayo ya nyuklia.../