Ulaya: Tutaendelea kuheshimu makubaliano ya nyuklia na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28480-ulaya_tutaendelea_kuheshimu_makubaliano_ya_nyuklia_na_iran
Kamishna wa Masuala ya Nishati wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, wanachama wa Umoja huo wataendelea kuheshimu makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 30, 2017 23:42 UTC
  • Ulaya: Tutaendelea kuheshimu makubaliano ya nyuklia na Iran

Kamishna wa Masuala ya Nishati wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, wanachama wa Umoja huo wataendelea kuheshimu makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA.

Miguel Arias Canete alisema hayo jana Jumapili mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran na huku akizungumzia kikao cha fikra za pamoja baina ya Iran na Umoja wa Ulaya kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa aliongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unafanya jitihada za kuhakikisha kuwa Iran inaondolewa vikwazo vyote.

Amesema, Iran ni mshirika mzuri wa Umoja wa Ulaya na ni sehemu nzuri ya kiuchumi katika eneo hili la Mashariki ya Kati. Ameongeza kuwa, Iran ina uwezo na mazingira mazuri ya kupunguza gesi hatari za "green house"na inaweza kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya muda mrefu ya kupambana na gesi hizo haribifu, katika eneo hili.

Makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa makubaliano ya JCPOA

 

Kamishina huyo wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya nishati amegusia pia maafikiano ya kulinda mazingira yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa, na kusisitiza kuwa, kwa mujibu wa makubaliano hayo, inabidi ifikapo mwaka 2020 kuwe kumepunguzwa asilimia 20 ya kuzalisha gesi hizo hatari, na mwaka 2030, uzalishaji wa gesi hizo uwe umepunguzwa kwa asilimia 40, na matumizi ya nishati safi yaongezeke kwa asilimia 30 kote ulimwenguni ifikapo mwaka huo.

Siku ya Jumamosi, ujumbe wa Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Miguel Arias Canete ulikuwa na kikao cha kibiashara na kibenki hapa mjini Tehran pamoja na kikao cha fikra za pamoja baina ya Iran na umoja huo kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.