Maonyesho ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi yaanza Tehran
Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Mafuta, Gesi, Petrokemikali na Vituo vya Kusafisha Mafuta ya Iran yameanza leo Tehran huku kukiwa na washiriki 4,000 wa kitaifa na kimataifa.
Mohammad Nasseri, Mkurugenzi wa maonyesho hayo anasema mwaka huu kuna mashirika 1,500 kutoka nchi 37 ambayo yanashiriki katika maonyesho hayo ya kimataifa.
Aidha amesema mashirika ya Ujerumani yakifuatiwa na ya Uchina ndiyo yaliyochukua nafasi kubwa zaidi katika maonyesho hayo huku nchi kama vile Italia, Uholanzi, Ufaransa na Uingereza nazo pia zikiwa na idadi kubwa ya mashirika.
Kati ya mashirika makubwa ya kimataifa ambayo yanashiriki katika maonyesho hayo ni pamoja na Total na British Petroleum.
Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Mafuta, Gesi, Petrokemikali na Vituo vya Kusafisha Mafuta ya Iran yanatazamiwa kuendelea hadi tarehe 9 Mei katika eneo la maonyesho ya kimataifa ya Tehran.
Iran ni kati ya nchi zenye hifadhi kubwa zaidi ya mafuta na gesi duniani na pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC na pia Jumuiya ya Nchi Zinazouza Kwa Wingi Gesi Duniani GECF.