Makamu wa Rais wa Iran ajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29188-makamu_wa_rais_wa_iran_ajiondoa_katika_kinyang'anyiro_cha_urais
Es'haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amejiondoa katika mchuano wa kuwania urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku moja baada ya wagombea wengine wawili wa kiti hicho kutangaza kujiondoa kwenye mchuano huo wa Ijumaa ijayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 16, 2017 23:22 UTC
  • Makamu wa Rais wa Iran ajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais

Es'haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amejiondoa katika mchuano wa kuwania urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku moja baada ya wagombea wengine wawili wa kiti hicho kutangaza kujiondoa kwenye mchuano huo wa Ijumaa ijayo.

Katika taarifa aliyotoa jana Jumanne, Jahangiri amesema baada ya mashauriano ya kina na wadau mbalimbali katika mrengo wa wapenda mageuzi, ameamua kujiondoa katika uchaguzi huo na badala yake ametangaza kumuunga mkono Rais wa sasa Hassan Rouhani.

Kadhalika katika taarifa hiyo ametoa wito kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo ili kulinda kile anachokitaja kama mjadala wa matumaini, amani, maendeleo na uwajibikaji.

Wagombea wengine wanaoripotiwa kujiondoa katika duru hii ya 12 ya uchaguzi wa rais wa Iran ni Mustafa Hashemi Taba ambaye Jumatatu alitoa taarifa na kusema atampa kura yake rais wa sasa Hassan Rouhani, huku Meya wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf, pia akijiondoa na kutoa wito kwa wafuasi wake kote Iran kumuunga mkono Ibrahim Raisi Sadat.

Rais Rouhani (kulia) na makamu wake Jahangiri

Wagombea wa urais waliosalia katika mchuano huo ni  Mostafa Aqa-Mirsalim ambaye ni waziri wa zamani wa utamaduni na muongozo wa Kiislamu, Sayyid Ebrahim Raisi, msimamizi wa Haram Takatifu ya Imam Ridha AS na Rais wa hivi sasa, Dakta Hassan Rouhani ambaye anatetea nafasi yake ili amalize kipindi chake cha pili.

Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi huu wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran.