Rouhani: Haram na matukufu ya Kiislamu ni mstari mwekundu kwa Iran
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haitoruhusu makundi ya kigaidi kushambulia Haram na matukufu mengine ya Kiislamu nchini Iraq na Syria huku akisisitiza kuwa, maeneo matakatifu ya kidini ni mstari mwekundu wa taifa hili.
Katika hotuba yake leo Jumamosi hapa mjini Tehran aliyoitoa kwa mnasaba wa Siku ya Mashahidi, Rais Rouhani amesema kuwa: “Haijalishi Haram hizo ziko wapi, iwe Syria, Iran au katika nchi yeyote ile, Iran haitoruhusu jaribio lolote la magaidi kuyahujumu maeneo matakatifu na Haram za watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad SAW.”
Rais wa Iran ameongeza kuwa, mashahidi wametufundisha kuwalinda ndugu zetu Waislamu na matukufu ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu iwapo yapo katika hatari ya kushambuliwa. Akizihutubia familia za mashahidi hao, Rais Hassan Rouhani amesema: "Watoto wenu wameonyesha kuwa walikuwa tayari kuilinda Iran, ardhi za Waislamu na Haram za Familia ya Mtume Mtukufu SAW popote pale walipo."
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma washauri wake wa kijeshi nchini Syria na Iraq kwa lengo la kuzisadia nchi hizo kuzuia hujuma dhidi ya haram tukufu. Baadhi ya washauri hao wameuawa shahidi katika hujuma za matakfiri wa Daesh.