Wananchi wa Iran leo wanashiriki katika uchaguzi wa Urais
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29270-wananchi_wa_iran_leo_wanashiriki_katika_uchaguzi_wa_urais
Wananchi wa Iran waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanaelekea katika masanduku ya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua Rais wa nchi.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
May 18, 2017 23:52 UTC
  • Wananchi wa Iran leo wanashiriki katika uchaguzi wa Urais

Wananchi wa Iran waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanaelekea katika masanduku ya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua Rais wa nchi.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran inayosimamia uchaguzi huo imetangaza kuwa, watu milioni 56 na laki nne na elfu 10 na 234 wametimiza masharti ya kupiga kura. 

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema asubuhi ya leo na tayari zoezi la upigaji kura limeanza. 

Licha ya kuwa kiti cha Urais kinawaniwa na wagombea wanne lakini mchuano mkali unatarajiwa kushudiwa kati ya Rais wa sasa Hassan Rouhani na Sayyid Ibrahim Raeisi, Msimamizi wa Haram ya Imam Ridha AS. rais Rouhani anatoka katika mrengo wa wapenda mageuzi huku Sayyid Ibrahim Raeisi akiwania kiti hicho kutoka mrengo wa wahafidhina. Wagombea wengine wa kiti cha Urais ni Mostafa Aqa-Mirsalim mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu na Makamu wa Zamani wa Rais wa Iran, Mostafa Hashemi-Taba.

Wairani nje ya nchi wakishiriki katika uchaguzi wa leo

Wairani wanaoishi nje ya nchi pia wana fursa ya kushiriki katika uchaguzi wa leo baada ya kuwekwa vituo 55 vya kupigia kura nchini Marekani, 21 nchini Imarati, 22 nchini Iraq na 12 nchini Uingereza.

Uchaguzi wa leo wa rais nchini Iran unafanyika ambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji na uchaguzi mdogo wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).