Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran kufunguliwa
Maonyesho ya 25 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran yanaanza leo Alasiri katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA mjini Tehran.
Taarifa zinasema maonyesho hayo ya kimataifa yatahudhuriwa na taasisi 50 na pia kutakuwa na mashirika zaidi ya 297 ya uchapishaji. Kati ya mashirika hayo, 281 ni kutoka Iran na 16 ni ya kimataifa kutoka nchi kama vile Uturuki, Iraq, Lebanon na Syria.
Mkurugenzi wa maonyesho hayo Abbas Nazarirad amemwambia mwandishi wa IQNA kuwa, maoneysho hayo yataendelea kwa muda wa siku 18.

Aidha amesema kuwa milango ya maonyesho hayo itakuwa wazi kila siku kuanzia saa 12 jioni hadi saa sita usiku.
Afisa huyo amedokeza kuwa, nara ya maonyesho ya mwaka huu ni "Qur'ani, Maadili na Maisha" na kwamba kutakuwa na hafla kadhaa kuhusiana na mada hii. Aidha mwaka huu kutakuwa na maonyesho maalumu yenye anwani ya: "Robo Karne ya Harakati za Qur'ani" ambapo washiriki watabainishiwa mafanikio ya maonyesho hayo ya kimataifa ya Qur'ani katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.