Kermani: Kushikamana na Uislamu na Qur'an ndio mafanikio ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30556-kermani_kushikamana_na_uislamu_na_qur'an_ndio_mafanikio_ya_iran
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo mjini Tehran, Ayatullah Muhammad Ali Muvahhedi Kermani amesema kuwa, Marekani ndiye adui mkuu wa taifa la Iran na kwamba, kushikamana na misingi ya dini ya Uislamu na Qur'an Tukufu ndiko kulikoiwezesha Jamhuri ya Kiislamu kusimama imara mbele ya Marekani na maadui wengine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2017 10:57 UTC
  • Kermani: Kushikamana na Uislamu na Qur'an ndio mafanikio ya Iran

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo mjini Tehran, Ayatullah Muhammad Ali Muvahhedi Kermani amesema kuwa, Marekani ndiye adui mkuu wa taifa la Iran na kwamba, kushikamana na misingi ya dini ya Uislamu na Qur'an Tukufu ndiko kulikoiwezesha Jamhuri ya Kiislamu kusimama imara mbele ya Marekani na maadui wengine.

Ayatullah Muhammad Kermani ameyasema hayo katika hotuba ya sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran ambapo sambamba na kubainisha kwamba, maslahi ya taifa la Iran yatafikiwa iwapo tu hayataenda kinyume na utambulisho wa Iran ya Kiislamu amesema kuwa, kutowategemea maadui, kutumia nguvukazi ya vijana na kutegemea uchumi wa kimapambano, ni mambo ambayo yanaweza kulifanya taifa hili kuendelea kusimama imara dhidi ya mashinikizo ya maadui.

Baadhi ya watawala wa Marekani wanaofanya njama chafu dhidi ya Iran ya Kiislamu

Kadhalika khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran ameashiria namna viongozi wa wa utawala wa Kiislamu wanavyopaswa kuwajali watu wenye hali ngumu, kujiepusha na anasa za kidunia na majingambo, kukubali kukosolewa, kuwa makini katika uteuzi wa viongozi na pia uadilifu katika ugawaji mali na kusema kuwa, hayo ni katika mambo ambayo yanapaswa kushuhudiwa katika serikali ya Kiislamu kwa mtazamo wa Imamu Ali Bin Abi Twalib AS.

Katika sehemu nyingine ya khutba zake, Ayatullah Muhammad Ali Muvahhedi Kermani amewataka Waislamu kuzidisha uchaji-Mungu na kuitaja tarehe 21 ya Mwezi wa Ramadhani kuwa inakumbushia tukio la kuuawa shahidi Amirul-Muuminina Ali AS na kusisitiza kuwa, mtukufu huyo alikuwa ni kiumbe bora katika zama zake kutokana na fadhila na utukufu aliokuwa nao.

Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imamu Ali Bin Abi Twalib (as)

Itakumbukwa kuwa, Imam Ali bin Abi Talib AS Khalifa wa baada ya Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume alikufa shahidi tarehe 21 Ramadhan mwaka wa 40 Hijiria baada ya kupigwa upanga wenye sumu akiwa kwenye sijda katika Mihrabu siku mbili kabla. Ibn Muljim aliyekuwa mfuasi wa genge la Khawarij ndiye aliyempiga upanga wenye sumu mtukufu huyo na kumpasua utosini.