Iran yalaani hatua ya Marekani kutungua ndege yake ya abiria mwaka 1988
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani kitendo kilicho dhidi ya ubinadamu cha meli ya kivita ya Marekani kuitungua ndege ya abiria ya Iran Air Julai 3 mwaka 1988 na kuongeza kuwa Marekani inapaswa kuwajibika kuhusu jinai yake hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya hatua ya meli ya kivita ya Marekani kutungua ndege hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: Taifa la Iran linawatambua waliotenda jinai hiyo kuwa ni watu wasio na mantiki kwa kudai kuwa eti ni waungaji mkono wa haki za binadamu na kwamba, wanapaswa kuwajibika kuhusu vitendo vyao vilivyo dhidi ya ubinadamu.
Wizarar ya Mambo ya Nje ya Iran imesema, Marekani ina historia ndefu ya kuwaua watu wasio na hatia kote duniani wakiwemo watu madhulumu wa Iran ya Kiislamu. Taarifa hiyo imesema: Vitendo vilivyo dhidi ya ubinadamu ni sehemu ya utambulisho wa tawala mbalimbali za Marekani.

Taarifa hiyo imetolewa kwa mnasaba wa siku kama hii ya leo miaka 29 iliyopita wakati ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege la Iran Air iliyokuwa ikitokea mji wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran kuelekea Dubai, iliposhambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo.
Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama na ugaidi unaotekelezwa na serikali ya Marekani. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao huo pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho cha kigaidi.