Iran yajitosheleza kuzalisha makombora, mabomu erevu, drone
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejitosheleza katika kuzalisha silaha za aina mbalimbali zikiwemo makombora, mabomu erevu na ndege zisizo na robani au drone.
Hayo yamedokezwa na Brigadier Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, IRGC. Ameongeza kuwa, hivi sasa pia Iran imejitosheleza katika uundaji wa rada, mfumo wa kujihami angani na vifaa vya vita vya kielektroniki.
Akizungumza Jumanne katika mkutano wa wabunge, amesema Iran imepata mafanikio makubwa sana katika sekta ya ulinzi. Aidha amesisitiza kuwa, uwezo mkubwa wa kijeshi wa Iran si tishio kwa nchi zingine kwani lengo la nchi hii ni kujihami na kumzuia adui.
Akiashiria shambulizi lililotekelezwa na IRGC hivi karibuni dhidi ya ngome za magaidi wa ISIS mkoani Dayr Ezzor nchini Syria, Hajizadeh amesema makombora yote yalipiga kwa kina maeneo yaliyokusudiwa.
Aidha ameashiria nafasi ya Marekani katika kuibua changamoto zilizopo Mashariki ya Kati na kusema: Hivi sasa Iran inakabiliana na mahasimu katika medani kadhaa za kivita.