Rais Rouhani: Iran na Chad zitaimarisha uhusiano wa pande mbili
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Chad katika nyuga mbalimbali.
Rais Rouhani ameyasema hayo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya Chad iliyoadhimishwa jana Ijumaa.
Katika ujumbe huo kwa Rais Idriss Déby wa Chad, Rais Rouhani amesema uhusiano wa pande mbili wa Tehran na N'Djamena uko katika kiwango cha kuridhisha na anatumai utaimarika zaidi.
Rais wa Iran sambamba na kumtakia kheri na fanaka mwenzake wa Chad na wananchi wa taifa hilo la Kiafrika katika maadhimisho ya miaka 57 ya uhuru, amesema ni katika sera za Iran kutoa kipaumbele kwa suala la kuimarisha ushirikiano na nchi za Kiafrika katika nyuga mbali mbali.
Miaka 57 iliyopita nchi ya Chad ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa na tarehe 11 Agosti hutambuliwa kama Siku ya Taifa nchini humo.
Mwezi Aprili mwaka jana, Rais Idriss Déby aliibuka mshindi wa uchaguzi wa rais na hivyo kupata fursa ya kuendelea kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa tano mfululizo.
Licha ya kugunduliwa akiba kubwa ya mafuta hapo mwaka 2006 nchini Chad, lakini idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo ya katikati mwa Afrika wanaishi katika hali ya umasikini mkubwa.