Iran kuzidisha himaya na uungaji mkono kwa harakati za muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33897-iran_kuzidisha_himaya_na_uungaji_mkono_kwa_harakati_za_muqawama
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili litaendelea kuyapa himaya na kuyaunga mkono makundi ya wanaharakati wa muqawama licha ya madola ya Magharibi kuitaka Tehran isiyaunge mkono makundi hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2017 02:51 UTC
  • Iran kuzidisha himaya na uungaji mkono kwa harakati za muqawama

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili litaendelea kuyapa himaya na kuyaunga mkono makundi ya wanaharakati wa muqawama licha ya madola ya Magharibi kuitaka Tehran isiyaunge mkono makundi hayo.

Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Alam jana usiku, Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema harakati za mapambano na muqawama zimejengeka katika mizizi ya utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba Iran itaendelea kuyaunga mkono kwa hali na mali.

Amesema: "Pengine madola ya kiistikbari ya Magharibi yanaogopa kuimarika uhusiano wa Iran na makundi ya muqawama kama Hizbullah yakihofia kusambaratika maslahi yao."

Brigedia Jenerali Amir Hatami amebainisha kuwa, neno 'muqawama' lina maana ya ulinzi mkabala wa uistikbari, ukatili na ukandamizaji na kwamba kwa mujibu wa mafunzo ya Uislamu, dini hii hairuhusu dhulma, ukandamizaji, maonevu na kuhujumiwa.

Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itazidisha uungaji mkono wake kwa harakati za mapambano na kwamba ni katika ajenda kuu ya Iran kuimarisha usalama wa taifa, na kuhakikisha kuwa ukosefu wa amani na usalama hauenei katika nchi za eneo na kote duniani kwa ujumla.

Matamshi ya Brigedia Jenerali Amir Hatami yameonekana kuwa radiamali kwa madai ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa Iran inaunda viwanda vya kutengeneza makombora nchini Lebanon, tuhuma ambazo zimekanushwa vikali na serikali ya Beirut kupitia Waziri Mkuu, Saad Hariri.