Wanachuo waandamana Tehran kuunga mkono Waislamu wa Myanmar
Wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu nchini Iran wamefanya maandamano mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Tehran na kuzitaka nchi za Kiislamu na jamii ya kimataifa hasa hasa Umoja wa Mataifa kutoendelea kunyamazia kimya mauaji ya kimbari wanayofanyiwa Waislamu wa Myanmar.
Waandamanaji hao wamelaani misimamo ya kindumilakuwili inayochukuliwa na jamii ya kimataifa kuhusu matukio ya kigaidi yanayotokea sehemu mbalimbali duniani na kusisitiza kuwa: Mjibizo (reaction) wa Umoja wa Mataifa kuhusu mashambulizi ya kigaidi ya mwezi Januari 2015 huko Paris Ufaransa ni tofauti kabisa na radiamali yake kuhusu mauaji ya Waislamu wa Yemen na Myanmar kwani siku moja tu baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi ya mjini Paris, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha dharura kuzungumzia mashambulizi hayo, lakini hadi hivi sasa umoja huo umekaa kimya mbele ya mauaji ya kutisha ya Waislamu wa Yemen na Myanmar.
Waandamanaji hao wamelaani jinai za serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya na kuitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na nchi za Kiislamu zinazopakana na Ghuba ya Uajemi kuchukua hatua madhubuti za kuwaokoa Waislamu hao.
Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu. Hadi hivi sasa maelfu ya Waislamu hao wameshauawa na kujeruhiwa na karibu laki tatu wengine wamekimbia makazi yao.
Serikali ya kibudha ya Myanmar inawanyima Waislamu hao hata haki zao za kimsingi kabisa kama vile uraia huku Marekani ikitangaza rasmi kuunga mkono jinai zinazofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu hao.