Rais Rouhani ataka serikali ya Myanmar isitishe mauaji ya kimbari ya Waislamu
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hali ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar ni ya kusikitisha huku akisisitiza udharura wa kuishinikiza serikali ya Myanmar ili isitishe mauaji ya kimbari na ukandamizaji dhidi ya Waislamu Warohingya.
Rais Rouhani ameyasema hayo mjini New York wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Stefan Löfven Waziri Mkuu wa Sweden pembizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa, Waislamu wa Myanmar wanakabiliwa na hali ngumu na kuongeza kuwa: "Umoja wa Ulaya unaweza kuwa na nafasi muhimu katika kusitisha ukandamizaji wa Waislamu wa Myanmar na kuwasaidia wakimbizi katika jamii hiyo."
Rais Rouani pia ameashiria mauaji ya idadi kubwa ya watu na maelfu kuwa wakimbizi kutokana na hujuma ya Saudia huko Yemen na kusema kuna ulazima wa kusitishwa mapigano haraka na kuanza mazungumzo baina ya pande hasimu.
Rais wa Iran pia amepongeza msimamo wa Sweden na Umoja wa Ulaya kwa ujumla kuhusu mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani na kusema msimamo wa utawala wa sasa wa Marekani kuhusu mapatano hayo si wa kimataifa.
Wakati huo huo, Rais Hassan Rouhani amekutana na kufanya mazungumzo na Antonio Guterres katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pembizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York. Katika mkutano huo Rais Rouhani ameashiria kadhia ya kura ya maoni ya eneo la Kurdistan, Iraq na kusema hatua yoyote ya kubadilisha mipaka ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati ni hatari.
Rouhani aidha amesema Iran iko tayari kuusaidai Umoja wa Mataifa kutatua matatizo ya eneo hilo na kusema mapatano ya nyuklia ya Iran ni mfano wa kuigwa katika utatuzi wa matatizo ya kieneo na kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Guterres ameunga mkono msimamo wa Iran wa kupinga kugawanywa Iraq vipande vipande na kusema, hatua kama hiyo inaweza kuvuruga amani katika eneo hilo. Aidha amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kushirikiana na Iran katika kurejesha amani na usalama wa kudumu Asia Magharibi.