Larijani: Iran itawafanya Wamarekani wajute
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35767
Spika Bunge la Iran amesema kuwa, iwapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran imetayarisha mipango ya kudumisha miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 17, 2017 15:13 UTC
  • Larijani: Iran itawafanya Wamarekani wajute

Spika Bunge la Iran amesema kuwa, iwapo Marekani itajiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran imetayarisha mipango ya kudumisha miradi yake ya kuzalisha nishati ya nyuklia.

Dakta Ali Larijani ambaye alikuwa akizungumza na kanali za televisheni za NTV na Russia-1 ameashiria uwezekano wa Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo na kusema: Mipango ya Iran ya kukabiliana na njama za Marekani iko wazi na Jamhuri ya Kiislamu itafanya mambo ambayo yatawafanya Wamarekani wajutie.

Kuhusu jibu la Tehran dhidi ya matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kadhia ya nyuklia, Spika Larijani amesema: Trump hana mamlaka yoyote ya kuthibitisha au kutothibitisha kwamba Iran imetekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hiyo ni kazi ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia ambao umethibitisha kwamba Iran imetekeleza majukumu yake. 

Image Caption

Spika wa Bunge la Iran amesema, mbali na Marekani, nchi nyingine kama Russia, China, Uingereza, Ujerumani na Umoja wa Ulaya zilishiriki katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na baada ya kufikiwa makubaliano kulitolewa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha makubaliano hayo. Amesisitiza kuwa Rais Donald Trump wa Marekani haelewi masuala ya kisheria na ni mwanagenzi katika masuala ya kisiasa. 

Licha ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kutangaza kwamba, Iran imeheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia maarufu ka kifupi kama JCPOA, Rais Donald Trump wa Marekani alidai hivi karibuni kwamba, Iran haijatekeleza makuabalino hayo, suala ambalo limekosolewa na kupingwa na hata waitifaki wa Magharibi wa serikali ya Washington.