Iran na Niger zasisitiza kukuza uhusiano wa kisiasa na kupambana na ugaidi
(last modified Fri, 27 Oct 2017 07:59:39 GMT )
Oct 27, 2017 07:59 UTC
  • Iran na Niger zasisitiza kukuza uhusiano wa kisiasa na kupambana na ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Rais wa Niger wamesisitiza suala la kukuza uhusiano wa kisiasa kati ya pande mbili na kupambana na ugaidi.

Muhammad Javad Zarif na Rais Mahamadou Issoufou jana usiku walikuwa na mazungumzo huko Niamey mji mkuu wa Niger ambapo walisisitiza kuimarisha uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara kati ya nchi mbili. Vilevile wamebadilishana mawazo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa na vita dhidi ya ugaidi. 

Kabla ya kufanya mazungumzo na Rais wa Niger, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikutana pia na Brigi Rafini, Waziri Mkuu wa Niger ambapo walizungumzia suala la kuimarisha na kuboresha ushirikiano wa pande mbili khususan ushirikiano wa kiuchumi, masuala ya kieneo na kimataifa.  

Waziri Zarif alishiriki pia katika ufunguzi wa jengo la biashara la pamoja kati ya Iran na Niger akiwa ameambatana na mwenyeji wake wa Niger, Ibrahim Yacouba baada ya kuonana na Rais wa nchi hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasili Niamey mji mkuu wa Niger alasiri ya jana. 

Muhammad Javad Zarif akiwa na waziri mwenzake wa Niger Ibrahim Yacouba mjini Niamey 

Kabla ya kuelekea nchini Niger, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa  amefanya ziara huko Uganda na Afrika Kusini na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo. 

Tags