Qassemi: Viongozi wa Saudi Arabia wanafanya njama za kuanzisha adui bandia
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kujadiliwa masuala ya pande mbili, kieneo, kimataifa, vita dhidi ya ugaidi na kupanua ushirikiano wa pande mbili ndizo ajenda kuu za kikao cha pande tatu cha viongozi wa Iran, Russia na Azerbaijan.
Bahram Qassemi amesema hayo leo katika kikao chake na waandishi wa habari wa ndani na wa nje na kueleza kuwa, kikao kijacho cha pande tatu cha viongozi wa Iran, Russia na Azerbaijan ni fursa muhimu mno kwa viongozi wa ngazi za juu wa nchi hizo ya kuweza kufanya majadiliano na mashauriano kuhusiana na masuala mbalimbali. Aidha Qassemi amesema kuhusu kikao kilichoanza leo mjini Astana, Kazkhstan cha kujadili mgogoro wa Syria kwamba, ana matumaini kutapatikana mwafaka unaotakiwa kati ya Iran, Russia na Uturuki ili ipigwe hatua moja mbele katika kuwasaidia wananchi wa Syria pamoja na amani na uthabiti wa eneo.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusiana na suala la Yemen kwamba, kadhia ya nchi hiyo iko wazi na mvamizi anaeleweka bayana na hata suala la kwamba, ni watu gani wanaotumia silaha nzito na kurusha mabomu katika maeneo ya makazi ya raia, nalo liko wazi.
Bahram Qassemi amesema, inaonekana kuropokwa na kubwabwaja imekuwa ila mbaya ambayo viongozi wa Saudia hawawezi kuiacha na kuongeza kuwa, viongozi wa Riyadh wamekuwa wakiyatafutia majibu matatizo yao kwa kuzusha fitina na kuwaingiza watu wengine katika mambo hayo.
Qassemi amebainisha kuwa, viongozi wa Saudia wanafanya njama za kuanzisha adui bandia na kueneza chuki dhidi ya Iran kwa njia yoyote ile, ingawa hadi sasa njama zao hizo zimegonga ukuta.