Jeshi la Anga la Iran laanza mazoezi makubwa kati mwa nchi
Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeanzisha mazoezi makubwa yanayojumuisha ndege aina mbali mbali za kivita katika eneo la Isfahan, kati mwa Iran.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Radio Tehran, Msemaji wa Mazoezi hayo ya Saba ya Nguvu za Anga za Waliojitolea Kulinda Anga ya Wilayat, Brigedia Jenerali Massoud Rouzkhosh amesema: "Mazoezi haya ya siku mbili yatajumuisha ndege aina mbali mbali za kivita, ndege za upelelezi, ndege za vita vya kielektroniki, ndege kubwa za kubeba na kujaza mafuta ndege za kivita zinazoruka angani na ndege zisizo na rubani au drone."
Aidha amesema mazoezi hayo yaliyoanza Jumatatu yanafanyika katika fremu ya mazoezi ya kila mwaka ya kuimarisha uwezo wa jeshi la anga la Iran katika masuala ya vita vya kawaida, vita vya kielektroniki na kufanyiwa majaribio rada na zana nyinginezo za kivita.
Kati ya ndege za kivita zinazoshiriki katika mazoezi hayo ni Sukho-24, F-4, F-5, F-7, F-14, MiG-29, na Sa’egheh au radi ambayo ni ndege iliyoundwa hapa nchini Iran.
Katika mkesha wa kuanza mazoezi hayo, Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami alizindua mfumo mpya wa rada unaojulikana kama Afaq ulotengenezwa na wataalamu wa hapa nchini.
Iran hufanya mazoezi makubwa ya kijeshi mara kwa mara ili kubaini uwezo na utayarifu wa vikosi vya ulinzi wa kuihami nchi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi yoyote ile bali sera zake za ulinzi zimejengeka katika msingi wa kujihami na kukabiliana na adui.