Rais Rouhani awasilisha pendekezo la kutatua mgogoro wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36667-rais_rouhani_awasilisha_pendekezo_la_kutatua_mgogoro_wa_syria
Rais Hassan Rouhani anayeshiriki kikao cha marais wa Russia, Uturuki na Iran katika mji wa Suchi amewasilisha pendekezo lenye vifungu vikuu vitatu kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Syria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 22, 2017 16:34 UTC
  • Rais Rouhani awasilisha pendekezo la kutatua mgogoro wa Syria

Rais Hassan Rouhani anayeshiriki kikao cha marais wa Russia, Uturuki na Iran katika mji wa Suchi amewasilisha pendekezo lenye vifungu vikuu vitatu kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Syria.

Dakta Hassan Rouhani amesema katika kikao hicho kinachofanyika Russia kwamba vita dhidi ya ugaidi bado haijamalizika na kwamba ushindi uliopatikana hivi karibuni dhidi ya kundi la Daesh haupaswi kuzighafilisha nchi zinazopambana na uozo huo kuhusu hatari ya magaidi wa kitakfiri na kiwahabi. Amesema kuwa hatua ya kwanza ya pendekezo lake ni kuwasaidia watu wa Syria kudumisha mapambano dhidi ya ugaidi sambamba na kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo. 

Katika hatua ya pili ya pendekezo lake, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, sasa hakuna kisingizo chochote cha kuwepo majeshi ya nchi za kigeni katika ardhi ya Syria bila ya ruhusa na mwafaka wa serikali halali ya nchi hiyo na kuongeza kuwa: Baada ya miaka kadhaa ya mapambano dhidi ya magaidi na waungaji mkono wao, watu wa Syria wana uwezo wa kutengeneza mustakbali wao wenyewe unaodhamini uhuru wa kimsingi wa wananchi na kuheshimu demokrasia na haki za kaumu zote za nchi hiyo.

Marais Rouhani, Putin na Erdogan

Kifungu cha tatu cha pendekezo la Rais Hassan Rouhani kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Syria kinasisitiza kuwa, mchango wa jamii ya kimataifa katika mustakbali wa Syria unapaswa kuandamana na kuwasaidia watu wa nchi hiyo kwa ajili ya kurejesha amani, kuondoa matatizo na mashaka yao na kuijenga upya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kujiepusha kuingia masuala yao ya ndani au kuwatwisha Wasyria matakwa kutoka nje. 

Rouhani, Suchi nchini Russia

Marais wa nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki wanakutana leo mjini Sochi nchini Russia katika mazungumzo ya pande tatu ya kujadili matukio ya eneo katika kipindi cha baada ya Daesh (ISIS).