Velayati: Palestina ni kadhia nambari moja ya Ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i38145-velayati_palestina_ni_kadhia_nambari_moja_ya_ulimwengu_wa_kiislamu
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa ameeleza kuwa Palestina inaendelea kuwa suala la kwanza linalouhusu Ulimwengu wa Kiislamu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 26, 2017 11:53 UTC
  • Velayati: Palestina ni kadhia nambari moja ya Ulimwengu wa Kiislamu

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa ameeleza kuwa Palestina inaendelea kuwa suala la kwanza linalouhusu Ulimwengu wa Kiislamu.

Dakta Ali Akbar Velayati ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu amesema leo katika kikao na waandishi wa habari kuwa hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kuitambua rasmi Quds (Jerusalem) kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na agizo la Rais wa nchi hiyo la kuuhamisha ubalozi wa Washington kutoka Tel Aviv hadi Baitul Muqaddas imeonyesha kuwa, dunia nzima hususan Waislamu wameguswa na suala hilo. 

Mshauri wa Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa ameongeza kuwa, kura nyingi zilizopigwa na nchi mbalimbali duniani katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa za kupinga kubadilishwa hali ya mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, zimedhihirisha mwamko na kuwa macho fikra za waliowengi duniani. Amesisitiza kuwa, kura hizo zimepigwa licha ya vitisho na hila zote zilizofanywa na Marekani. 

Kikao cha Baraza Kuu la UN kilichoidhinisha azimio la kupinga kutambuliwa mji wa Quds kama mji  mkuu wa Israel 

Katibu Mkuu  wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu amesema kuwa, Marekani haikupata hata kura moja ya ndio katika Baraza la Usalama kwa ajili ya kuubadlilisha mji mkuu wa Israel, hatua  iliyokosolewa na Wamarekani wenyewe wakisema kuwa ushawishi wa serikali ya nchi hiyo ndani ya Umoja wa Mataifa umepungua. 

Alhamisi ya tarehe 21 mwezi huu  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao na kuidhinisha azimio lililopigiwa kura za ndio 128 zinazopinga kubadilishwa utambulisho wa mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu licha ya vitisho vya Trump na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa kwamba Washington itazikatia misaada ya kifedha nchi ambazo zitalipigia kura ya ndio azimio hilo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo pia limetambua haki za Wapalestina kuhusu Quds.