Jan 04, 2018 02:35 UTC
  • Rouhani na Erdogan walaani msimamo wa US, Israel dhidi ya Iran

Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki wamekosoa vikali uchochezi na uungaji mkono wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa waandamanaji wanaofanya fujo na ghasia nchini.

Katika mazungumzo ya simu jana Jumatano na mwenzake Hassan Rouhani, Recep Tayyip Erdogan amesema Uturuki inathamini usalama na uthabiti wa Iran kuutazama kama jukumu lake.

Amesema Ankara kwa kipindi kirefu imekuwa ikikabiliana na propaganda chafu za vyombo vya habari vya Magharibi, na vilevile matamshi ya uingiliaji mambo yake ya ndani ya Rais Donald Trump wa Marekani na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Kadhalika Rais Erdogan ameeleza kuhusu hamu ya Uturuki ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga mbalimbali mwaka huu 2018.

Maandamano ya kuiunga mkono serikali Jumatano

Kwa upande wake, Rais Hassan Rouhani amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa Ankara na Tehran katika uga wa uchumi hususan uhusiano wa kibenki na matumizi ya safaru za nchi mbili katika mabadilishano ya bidhaa na huduma.

Kuhusu hali ya kisiasa inayotawala nchini hivi sasa, Rais Rouhani amesema polisi imefanikiwa kuzima ghasia na kurejesha utulivu katika miji iliyokuwa ikishuhudia maandamano ya fujo.

Aidha amekariri kauli yake ya hapo awali kuhusu uhuru wa watu kufanya maandamano ya amani nchini na kudai matakwa yao, lakini amesisitiza kuwa serikali haiwezi kufumbia macho uvunjifu wa sheria na watu wanaohatarisha usalama wa taifa.

Tags