Iran yaanza mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la Muhammad Rasulullah SAW
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo linaanza mazoezi makubwa ya kijeshi ya pamoja yaliyopewa jina la Muhammad Rasulullah SAW-5 katika maeneo ya oparesheni ya kusini na kusini mashariki na pia katika pwani ya Bahari ya Makran na Bahari ya Oman hadi Daraja 15 kaskazini mwa Ikweta.
Hayo yamedokezwa na Admeri Habibullah Sayari, Mratibu Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alipokuwa akizungumza na waandishi habari na kuongeza kuwa: "Lengo la duru hii ya Mazoezi ya Muhammad Rasulullah SAW-5 ni kuinua uwezo na ustadi wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kutathmini uwezo wa kiharakati na ushirikiano wa vikosi vyote vya jeshi na pia kuinua kiwango cha mipango ya mazoezi ya pamoja."
Admeri Sayyari ameongeza kuwa ujumbe wa mazoezi hayo ya kijeshi ni ujumbe wa amani na urafiki kwa nchi jirani. Halikadhalika Mratibu Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebaini kuwa, "Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linaweza kudhamini usalama wa maji yote yaliyoko chini ya satwa yake na linaweza kulinda njia zote za kusafirishia nishati pamoja na kuhakikisha kuna usalama endelevu katika eneo."
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya ulinzi huku ikijitosheleza kwa kiasi kikubwa katika zana za kujihami. Aidha Jeshi la Iran hufanya mazoezi ya mara kwa mara kwa ajili ya kubaini uwezo wa vikosi vyake na pia kufanyia majaribio zana mpya za kivita. Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi zingine bali sera yake ya ulinzi imejengeka katika msingi wa kujihami.