Je, Trump yuko pamoja au dhidi ya watu wa Iran?
Rais Donald Trump wa Marekani katika hotuba yake ya kila mwaka mbele ya Bunge la Kongresi la nchi hiyo, kwa mara nyingine tena amedia kuwa eti yuko pamoja na watu wa Iran.
Katika hotuba yake hiyo, Rais wa Marekani baada ya kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amedai kuwa Marekani iko pamoja na watu wa Iran katika mapambano yao eti ya kupigania uhuru."
Trump aidha ameitaka Kongresi ya Marekani ifuatilie kile alichokitaja kuwa ni, "dosari za kimsingi katika mapatano mabaya ya nyuklia na Iran." Kabla ya hapo pia, wakati wa machafuko ya hivi karibuni katika baadhi ya maeneo ya Iran, Trump alitoa hotuba au kutuma ujumbe kupitia Twitter mara kadhaa ambapo alidai kuwa anawaunga mkono wananchi wa Iran. Lakini mtawala huyo huyo, katika wiki yake ya kwanza ya kushika hatamu za uongozi, alitia saini dikrii ya kuwazuia Wairani kuingia Marekani pasina kujadili itikadi zao za kidini au kisiasa. Wakati amri hiyo tata ilipoanza kutekelezwa, mamia ya Wairani walikwama katika viwanja vya ndege vya Marekani pamoja na kuwa walikuwa wamefika nchini humo kuonana na familia zao. Idadi kubwa ya Wairani hao pia walikamatwa na kudhalilishwa na maafisa wa usalama wa Marekani. Miongoni mwao alikuwa mtoto wa umri wa miaka mitano ambaye alikamatwa na maafisa wa uhamiaji. Hivyo, hata huyo mtoto mdogo ambaye alikuwa ameenda Marekani kufanyiwa upasuaji wa dharura mjini New York hakusalimika na alizuiwa kufika hospitalini ili kupata matibabu.
Mwezi Septemba mwaka jana pia, Rais wa Marekani, kabla ya hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alilitaja taifa la Iran kuwa ni 'taifa la kigaidi." Katika hotuba yake hiyo mbali na kuuvunjia heshima mara kadhaa mfumo wa kisiasa wa Iran pia alitumia jina bandia la Ghuba ya Kiarabu katika kutaja eneo la Ghuba ya Uajemi. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa rais wa Marekani kutumia jina hilo bandia kutaja Ghuba ya Uajemi ambayo kwa miaka zaidi ya elfu tatu ilipata umashuhuri duniani kama Bahari ya Pars.
Aidha Rais Trump wa Marekani ametoa vitisho mara kadhaa akisema atatupilia mbali mapatano ya nyuklia ya Iran na madola sita makubwa duniani ambayo ni Marekani yenyewe, Uingereza, Ufaransa, Russia, China pamoja na Ujerumani. Mtawala huyo wa Marekani amesema atabatilisha mapatano hayo yaliyoidhinishwa na serikali iliyopita ya Marekani na pia amesema atatekeleza vikwazo vilivyosimamishwa dhidi ya Iran.
Ikumbukwe kuwa vikwazo hivyo vya nyuklia dhidi ya Iran vilipelekea wananchi wa Iran wakumbwe na matatizo kwani nchi hii haikuweza kupata fedha zake baada ya kuuza mafuta katika soko la kimataifa. Vikwazo hivyo vilipelekea watu wengi wakose dawa na matibabu pamoja na matatizo mengine. Pamoja na hayo taifa shupavu la Iran lilifadhilisha kustahamili vikwazo hivyo ili kupata haki yake isiyopingika ya kumiliki teknolojia ya nuklia kwa malengo ya amani.
Pamoja na hayo, vitisho vya kuirejesha Iran katika kipindi cha kabla ya mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 ni jambo litakalowaathiri vibaya watu wote wa Iran. Hii ni kweli hasa kwa kuzingatia kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA , umesisitiza mara kadhaa kuwa Iran imefungamana na mapatano hayo ya nyuklia ambayo ni mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA.
Kwa kuzingatia historia hiyo fupi ya utawala wa Trump na tawala zingine zilizotangualia za Marekani, ni vigumu bali hata haiwezekani kukubali madai yao kuwa, eti wako pamoja na watu wa Iran.
Trita Parsi mwanzilishi wa Baraza la Kitaifa la Wairani Marekani anasema: "Bw. Trump, wewe hauko pamoja na watu wa Iran wakati unapowazuia kukutana na jamaa zao Wamarekani."